Wednesday, May 29, 2013

Je katiba itambue vazi rasmi la Rais?

Ndugu msomaji wa blog hii je unafahamu kuwa katika mihimili mitatu ya Serikali, ni mhimili mmoja tu ambao hauna vazi rasmi? Spika wa bunge ana vazi rasmi na hulivaa kwenye hafla mbali mbali za kiserikali, Jaji Mkuu ana vazi rasmi pamoja na Mwanasheria mkuu wa serikali, lakini je ni vazi gani rasmi huvaa Rais wa nchi? Suti tu inatosha hata kwenye sherehe ya kuapisha Rais mpya hakuna vazi wanalobadilishana kama ishara ya mabadiliko ya serikali? Nipe maoni yako.

Mabaraza ya ardhi yapingwa bungeni

Wabunge walihoji utendaji kazi wa mabaraza ya ardhi na kusema kwamba hauridhishi. Hoja kubwa ilikuwa kwamba, lengo la kuundwa kwa mabaraza ya ardhi ni kupunguza mlundikano wa kesi katika mahakama za kawaida lakini imeonekana kwamba mkakati huo umeshindwa kufanya kazi na badala yake mabaraza yameongeza mlolongo wa mashauri.

Pia lengo la kuundwa kwa mabalaza ilikuwa ni kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya usuluhishi (mediation) lakini taratibu zinazoendelea kwenye mabaraza ni sawa kabisa na mahakama za kawaida hivyo kuhoji umuhimu wa kuwepo kwa mabaraza ya kata.

Akijibu hoja hiyo Waziri wa ardhi Prof. Anna Tibaijuka alisema wizara inaendelea kuboresha utendaji kazi wa mabaraza hayo ikiwa ni pamoja na kurekebisha utaratibu wa upatikanaji wa wenyeviti wa mabaraza hayo.